SAIKOLOJIA : JE UNAJUA NAMNA YA KUTUMIA MUDA VIZURI?

Zamani niliwahi kusoma kisa cha mfalme mmoja aliyeitwa Mautiktiki. Sikumbuki alikuwa wa taifa gani. Nadhani alikuwa myunani wengine husema mgiriki.

Mfalme Mautikitiki alikuwa mtu aliyependa sana kufanya kazi mbalimbali za maendeleo ya watu wa miliki yake. Siku moja ungemkuta anajenga daraja siku nyingine anaonekana anajenga bohari la kuwekea akiba ya chakula cha jamii au anatayarisha barabara na shughuli nyingine nyingi.

Hata hivyo, kulikuwa na kitu kimoja kilichokuwa kikimsumbua sana. Siku zote asubuhi jua lilipochomoza aliongoza kikosi chake cha kazi kwenda kuanza kazi fulani, lakini kadri walivyofanya kazi jua lilikuwa likipanda juu hadi likaonekana liko sawa na kichwa.

Baada ya hapo jua huanza kutelemka kwa kasi huku Mfalme Mautikitiki akiwahimiza watumishi wake kuongeza juhudi ili kukamilisha kazi yao kabla halijatua. Jua linapotua na giza kuingia mfalme na kikosi chake hulazimika kuacha kuendelea na kazi hadi siku nyingine.

Jambo hili lilikuwa likimkera sana hata akalichukia jua. Siku moja akaamua watumishi wake watengeneze kamba kubwa na ndefu ili wairushe juu na kulifunga jua ili wawe wakilizuia kutua hadi wakamilishe kazi yao.

Siku kamba ilipokamilika, Mfalme na wasaidizi wake walianza safari alfajiri kwenda kulitafuta jua wakiamini wangelikuta bado liko chini ili walinase na kulifunga. Lakini kila wapofika mahali walikoliona hawakulikuta ila waliliona liko mbele mbali zaidi na limepanda juu. Siku nyingine wakaamua kuelekea upande linakoonekana likitua ili walikute chini na kulifunga kamba. Lakini huko pia hawakulikuta chini, bali lilionekana bado lingali liko juu na linaendelea kutua.

Mfalme Mautikitiki aliwaongoza watumishi wake mara nyingi kujaribu kulikamata jua lakini hawakuweza hadi mwisho akakata tamaa.

Masikini hakujua kuwa jua halikuwa likienda bali lilikuwa limetulia mahali pamoja.

Na kinachozunguka ni dunia.
Pia hakujua kuwa ingawa jua lilikuwa likionekana kama liko karibu lakini lilikuwa mbali sana na hakuna kiumbe yeyote anayeweza kulifikia na hata kama angethubutu angeungua wakati akiwa mbali sana kwa sababu lenyewe ni moto mtupu.

Kisa hiki cha kale kinahusiana na mada yagu ya wiki hii inayosema “Je unajua jinsi ya kutunza muda? Mfalme Mautikitiki alikuwa ana kazi nyingi alizotaka kuzifanya ziku zote katika maisha yake. Lakini aligundua kuwa wakati ulikuwa kikwazo kwake.

Kwa kuwa katika zama zake hapakuwa na elimu kuhusu sayari yeye aliamua kulikamata jua ili alizuie lisiende kasi na kumkwamisha kukamilisha kazi zake za kila siku.

Hebu jiulize maswali mawili. Je kama wewe ungeombwa kumshauri Mfalme Mautikitiki kuhusu changamoto hii iliyomkabili ungemshauri ufanye nini? Je wewe katika maisha yako unakabiliwa na changamoto kama hii iliyomkabili mfalme huyu? Yaani unajikuta una mambo mengi unayotaka kuyafanya katika siku lakini unapungukiwa na muda. Je ule ushauri ambao unafikiria ungempatia Mfalme Mautikitiki unaweza kuutumia kuutumia wewe ukakufaa? Au wewe hauna kabisa tatizo kama hilo; yaani unajiona una muda mwingi wa kufanya shughuli zote unazofikiria kuzifanya. Hebu kabla hatujaendelea tujiulize muda ni nini.

Muda ni nini?
Mjukuu wangu aliyezoea kunitegea vitendawili siku moja alinitegea kitendawili kinachosema. “Ni kitu gani kirefu kuliko vyote lakini pia ni kifupi kuliko vyote?” Aliponiona nimeduwaa na ninashindwa akaongeza maelezo haya, “Ni kitu kinachokwenda kasi kuliko vyote lakini pia huweza kwenda taratibu kuliko vyote” Ingawa bado nilikuwa sijaelewa ni kitu gani hicho lakini wakati nahangaika kufikiri nikagundua kuwa kitu hicho ni muda.

Mjukuu wangu akanipongeza kwa kupata jibu sahihi.
Muda ni mrefu kwa kuwa ndicho kipimo kinachotumika katika historia kueleza ni lini jambo fulani lilitokea kama vile tunavyojiuliza kwa mfano ni lini Tanzania Bara ilipata uhuru.

Hakuna kitu kinachoweza kutuonyesha ni wakati gani jambo hilo lilitokea isipokuwa kutaja mwaka.

Tunapotaja mwaka huo pia tunaweza kwa kutumia idadi ya miaka kujua ni muda gani umepata tangu wakati huo. Lakini pia unaweza kujiuliza ni wakati gani ulipolinunua gazeti hili unalolisoma.

Huenda sasa unapolisoma gazeti hili ni saa 4 na ulilinunua saa 2 au saa 3. Hivyo muda tangu ulipolipata gazeti hili ni saa 1 au 2. Muda ni kitu kifupi kuliko vyote kwa sababu hakuna mtu anayeweza kumaliza majukumu yote anayotakiwa kufanya katika maisha yake yote.

Muda huonekana unakwenda kasi kwa wale wenye maisha ya furaha na wasio na shida.

Lakini kwa wale wenye shida na matatizo muda huonekana unakwenda taratibu.

Tumeeleza sifa za muda, lakini bado hatujaeleza maana halisi ya muda. Muda ni kitu cha dhahania kwani huweza kuuona wala kuukamata. Ni kipindi cha wakati maalumu.

Kipindi hicho hupimwa kwa sekunde, dakika, siku, majuma, miezi, miongo, karne na milenia.

Tunawezaje kutunza au kusimamia Muda?
Muda ni kitu muhimu sana katika maisha ya binadamu ndiyo maana kuna misemo katika lugha zote duniani inayoonyesha umuhimu wa muda. Misemo ya kiswahili ni kama vile ‘wakati ni mali’, muda ni zaidi ya mali’, muda ndiyo maisha yetu’, wakati haumngoji mtu na mingine kadhaa wa kadhaa.

Vile vile kuna misemo inayohusu muda au wakati ambayo watu wamezoea kuitumia kama vile sina muda na kuchezea, usinipotezee wakati wangu, chunga wakati wako na mingine kadhaa.

Misemo yote hii inatufundisha jambo moja kubwa ambalo ni kwamba tunapaswa kutunza wakati na wala tusiupoteze bure kuutunza muda sio kuuchukua na kuuhifadhi mahali fulani kama vile sandukuni au chumbani, bali ni kuutumia vizuri kwa sababu wenyewe haukamatiki, hauonekani wala huwezi kuununua ili uuhifadhi kwa wingi na kuutumia siku utakapohitaji.

Jambo jingine muhimu la kukumbuka ni kwamba hatuwezi kufanya kama yule mfalme niliyemsimulia katika kisa cha mwanzoni mwa makala hii, aliyetaka kulifunga jua ili alidhibiti lisinde kasi na limngojee amalize kazi zake.

Katika ulimwengu wa leo kufanya hivyo ni kama kuisimamisha saa kwa kujidanganya kuwa ikisimama na muda utakuwa umesimama. Muda hausimami wala haumugojei mtu.

Kuna wakati nilifanya utafiti mdogo ili kutambua watu wana hisia gani kuhusu muda. Nilipowauliza watu kama wana muda wa kutosha nilipata majibu ya aina mbili. Kwa mfano mtu mmoja alisema “Mimi sina tatizo la muda.

Nina muda wa kutosha” lakini wakati huo huo kuna mtu mwingine anasema; Mimi sina muda wa kutosha.

Nina hangaika wala sijui nifanyeje;
Tunapozichunguza taarifa hizi za watu wawili zinazotofautiana tunapata swali moja kubwa. Wote tunafahamu kuwa siku huwa na saa 24 yaani 12 za mchana na 12 za usiku na ndizo ambazo kila mtu anazo. Sasa inakuwaje mtu mmoja mwenye fursa sawa na watu wengine anasema yeye hana muda wa kutosha na mwingine mwenye fursa kama yeye anasema yeye ana shida kwa sababu anapungukiwa muda.

Tofauti hizi zinaweza kuwa na mitazamo kama ifuatayo. Yule anayesema ana muda wa kutosha huenda ni mtu anayeishi bila kuwa na malengo na wala haangalii hatima ya maisha yake. Huyu anajidanganya tu. Kwa hakika hana muda ila hajui nini wajibu wake katika maisha yake na ni mambo gani anapaswa kufanya kwa ajili ya maendeleo yake binafsi, familia yake na jamii kwa ujumla. Huyu anastahili kuwa na stadi sio ya kutunza muda pekee bali ajengewe uwezo wa kuwa na upeo wa kufikiri na kutambua mambo anayopaswa kufanya kwa ajili ya maendeleo yake binafsi, ndugu na jamaa zake na jamii kwa ujumla.

Kwa yule anayesema hana muda wa kutosha anaweza kuwa katika mwelekeo sahihi wa maisha lakini pia anaweza kuwa amepotoka. Tunaweza kusema yuko katika mwelekeo mzuri kama atakuwa amejiwekea malengo ya maendeleo katika maisha yake na hivyo anafanya kila jitihada kutekeleza yale mambo yote yatakayomfikisha kwenye malengo na ndiyo maana anapungukiwa muda wa kufanya yote hayo. Lakini kama nilivyosema mtu anaweza kuwa anapungukiwa muda kwa dhamiri potovu. Yaani hana muda wa kutosha kwa kuwa anatumia muda wake mwingi kwa kufanya mambo yasiyo na manufaa kwa maisha yake.

Huenda yeye ni mfanyakazi; mara tu anapotoka kazini anajitumbukiza katika mambo ya starehe na anasa. Anakwenda kwenye mabaa, vilabu vya usiku na pengine hata kwenye majuba ya kamari yaani makasino. Anakaribia kukesha akiwa huko hata anakosa hata muda wa kulala. Kwa shughuli kama hizi mtu huyu anautumia muda wake vibaya.

Lakini kutumia muda vibaya hakuishii katika mtu kujivinjari katika starehe na burudani. Kuna watu wengine ambao wanaharibu maisha yao kwa kutokuutumia muda kabisa kwa kufanya kazi yoyote. Hawa ni watu wazembe. Wanalala zaidi kuliko kuwa macho na hata wanapokuwa macho wanakwenda kijiweni kupiga soga bila kufanya kazi yoyote.

Tujifunze kuutunza muda kwa kuutumia vizuri kwa kufanya mambo yenye manufaa kwetu binafsi, wale walio karibu nasi na jamii kwa ujumla.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata