NYARAKA ZA LISSU KUHUSU MADINI ZAMKUNA BASHE.

MBUNGE WA NZEGA MJINI, HUSSEIN BASHE.

MBUNGE wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), ameeleza kukunwa na nyaraka na maandiko ya Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, yanayohusu madini ya Tanzania.

Akichangia mjadala wa mapendekezo ya bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha bungeni mjini hapa jana, Bashe alisema kuwa baada ya kusoma maandiko hayo hadi usiku mnene, alibaini Tanzania imeibwa vya kutosha kwenye sekta hiyo.

“Jana (juzi) wakati Lissu nilienda kumwomba anipe yale maandiko yake na alinipa… nimeyasoma sana na hadi saa tisa usiku nilikuwa nayasoma maandiko yale," Bashe alisema.

"Ukisoma maandiko ya Jaji Bomani na kesi ambayo yeye Lissu aliisimamia mwaka 2006, nchi hii imeibiwa kwa muda mrefu sana.

Bunge limefanya makosa na huko nyuma tumefanya makosa, sasa tumepata mtu (Rais John Magufuli) wa kupambana na rasilimali za nchi hii tumuunge mkono Watanzana," alisema.

Alisifu jitihada za Rais Magufuli katika kulinda rasilimali za umma hasa madini na kuwaomba wabunge na Watanzania wote wamuunge mkono.

Bashe alisema kwa kuwa Rais ndiye mlinzi mkuu wa rasilimali za taifa, kuna umuhimu kwa kila Mtanzania kuona kuwa vita hii inamhusu badala ya kumwachia Rais Magufuli peke yake.

Bashe alimtaka Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Medad Kalemani, aliambie Bunge jinsi serikali itakavyozipata Sh. bilioni 10 ambazo kampuni hiyo iliondoka nazo.

“Mimi natoka Nzega, sasa kama Mbunge wa Nzega Mjini, naliambia Bunge kuwa tumeibiwa, tumeibiwa sana na kama alivyosema (John) Heche (Mbunge wa Tarime Vijijini -Chadema) jana (juzi), na mimi narudia leo (jana), Resolute wameondoka na fedha za 'Service Levy', lakini Kampuni yake tanzu imepewa leseni, mimi sitajali matokeo, nitawaongoza wananchi wangu kubomoa mabati ya chuo cha serikali,” alisema Bashe.

Alisema wawekezi hao wa madini wameacha mahandaki yenye urefu wa zaidi ya mita 1,000 ambayo walielezwa kuwa yatajaa maji baada ya miaka 200.

Bashe alisema pamoja na wizi uliofanywa na kampuni ya Resolute kwa kuondoka na fedha za halmashauri, kampuni yake tanzu imepewa leseni ya kupata maeneo ya uchimbaji maeneo hayo hayo ya Nzega.

Alisema Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Khamis Kigwangalla, alipigwa na kuumizwa alipokuwa akipambana kutaka wananchi wake wapate haki yao kwenye mgao wa madini, lakini alionekana hana maana.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata