BAADA YA DODOMA KIBAHA NAO WAPIGA MARUFUKU ULAJI WA KITIMOTO.

Halmashauri ya mji wa Kibaha kupitia Idara ya mifugo na uvuvi imepiga marufuku ulaji na uuzwaji wa nyama ya nguruwe baada ya kutokea mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nguruwe.

Afisa habari wa halmashauri ya Kibaha, Innocent Byarugaba amesema katazo hilo ni pamoja na kuzuia shughuli zote za uchinjaji wa nguruwe, kuingiza au kutoa nyama ya nguruwe katika maeneo yote ya  halmashauri ya Kibaha.

Byarugaba amesema katazo hilo ni kwa mujibu wa sheria namba 17 ya magonjwa ya mifugo ya mwaka 2003 na kuwa wamezuia uuzaji wa nyama hiyo ili kupunguza kasi ya ueneaji na usambaaji wa ugonjwa huo hadi hapo ugonjwa huo utakapodhibitiwa katika halmashauri hiyo.

Byarugaba amedai awali katika ufuatiliaji na  uchunguzi wa magonjwa ya mifugo ilibainika kuwepo kwa vifo vingi vya  nguruwe  mwanzoni mwa mwezi Mei katika baadhi ya  kata za mji wa kibaha.

Amesema  idara ya mifugo na uvuvi   kupitia wataalam wake baada ya kufanya uchunguzi walibaini dalili za ugonjwa wa homa ya nguruwe ambapo  walichukuwa sampuli mbalimbali za nguruwe waliokufa na kupeleka maabara ili kuthibitisha ugonjwa husika.

Mbali na hilo Byarugaba ametaja kata zilizoathirika zaidi  na ugonjwa huo kuwa ni Picha ya ndege na viziwa ziwa eneo la mikongeni ambapo jumla ya nguruwe 71  walikufa kutokana na ugojwa huo kuanzia mwezi Mei, na kuwa halmashauri hiyo ina jumla ya nguruwe  1328 kwa mujibu wa takwimu za mwezi Aprili mwaka huu.

Amezitaja dalili za nguruwe mwenye ugonjwa huo kuwa ni pamoja na kuvuja na kusambaa kwa damu kwenye mwili wa mnyama, homa kali, kupumua kwa shida, vifo vya nguruwe ndani ya siku mbili hadi kumi nakutapika.

Pia nyama ya nguruwe mwenye ugonjwa huo huonekana imevilia damu katika viungo mbalimbali baada ya kumpasua na dalili nyingine ni mimba kuharibika endapo mnyama atakuwa ana mimba.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata