ARUSHA: MAONYESHO YA KILIMO BIASHARA KUSHIRIKISHA ZAIDI YA WAKULIMA 3000

Wakulima zaidi ya 3000 wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, wanatarajiwa kushiriki maonyesho ya kilimo biashara, ambayo yameandaliwa na Baraza la Nafaka la Afrika ya Mashariki (EAGC).

Akizungumza na waandishi wa habari leo (Jumapili) Meneja wa Baraza wa EAGC, Ikunda Terry amesema maonyesho hayo, yatafanyika kuanzia Juni 29 hadi 30, katika viwanja vya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Seliani (SARI).

Terry amesema lengo la maonyesho hayo, ambayo pia yatahusisha mashirika zaidi ya 14 ya kimataifa, yakiwepo mabenki ni kusaidia ubunifu katika kilimo ili kuendana na kauli mbiu ya Tanzania ya Viwanda.

“Tunataka wakulima nchini, waongeze uzalishaji kwani bila kuongeza uzalishaji ni wazi viwanda ambavyo vitajengwa vitakosa malighafi,”amesema.

Amesema kauli mbiu ya maonyesho ya mwaka huu ni uvumbuzi na ubunifu kwenye kilimo biashara ili kuendana na mapinduzi ya viwanda.

Kaimu Mratibu wa Utafiti wa SARI, Rama Ngatoluwa amesema maonyesho hayo pia yanatarajiwa kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji wenye tija na kuhakikisha kuna usalama wa chakula.

Ngatoluwa, hata hivyo amesema changamoto kubwa inayowakabili wakulima wengi ni kutopata mbegu bora kwa wakati na pia bado mbegu bora ambazo zimefanyiwa utafiti zinauzwa bei ya juu.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya IFFA Seeds Ltd, Mohamed Ahmed amewataka wakulima kujitokeza kwa wingi kwenye maonyesho hayo ili kuona aina mbalimbali ya mbegu ambazo zimefanyiwa utafiti ili kuongeza uzalishaji.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata