KAMANDA KOVA ASTAAFU AOMBA TENA KAZI YA MASOKO JESHI LA POLISI

Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Polisi, Suleiman Kova, ameliomba jeshi hilo kumpa kitengo cha masoko ili aweze kulitangaza na kuliunganisha na wananchi, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa maboresho ndani ya jeshi hilo katika kukabiliana na uhalifu.

Kova alitoa ombi hilo jana mjini Moshi katika hafla fupi ya kumuaga iliyofanyika Shule ya Polisi Moshi (MPA).

Alisema jeshi hilo linaelekea kuzindua mpango wake wa matokeo makubwa sasa (BRN) ,ambao unahitaji msukumo wa jamii katika kusaidia kukabiliana na uhalifu wa aina mbalimbali ukiwamo wa mtandaoni na dawa ya kulevya.

Kova alisema kutokana na utumishi wake wa zaidi ya miaka 40 kwa kushirikiana na wastaafu wengine, wanaweza kusaidia na kuwa kiunganishi baina ya polisi na raia kama njia bora ya kukabiliana na uhalifu kwa kutumia kitengo cha masoko.

“Nimekuwa mtumishi ndani ya polisi kwa miaka 40, ninaweza kutumika hata na Shule ya Polisi Moshi kufundisha na hata kutoa uzoefu wangu ambao utalisaidia jeshi katika kukabili uhalifu, kama mnavyoniona ninazo nguvu za kutosha na ninalipenda Jeshi la Polisi,” alisema.
Katika hatua nyingine, Kamishna Kova aliiomba serikali kuliboresha zaidi jeshi la polisi kwa vifaa, mbinu na teknolojia za hali ya juu ili kukabiliana na matukio ya uhalifu wa aina mbalimbali unaokuwa kulingana na ukuaji wa teknolojia duniani.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata