HII HAPA HOTUBA YA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2016/2017

HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHE. DKT. PHILIP I. MPANGO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI TAARIFA YA HALI YA UCHUMI
2015 NA MPANGO WA MAENDELEO
WA TAIFA 2016/17
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa Mwaka 2015 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17. Pamoja na hotuba hii nawasilisha vitabu vya Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa Mwaka 2015 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17. Taarifa ya Hali ya Uchumi na Mpango ninayowasilisha ndio msingi wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/17. 

2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuendelea kushiriki Mkutano wa Tatu wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tukiwa na afya njema, amani na utulivu. Napenda kutumia nafasi hii pia kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha majadiliano ya Mpango wa Maendeleo kwa umakini na umahiri mkubwa tangu ngazi ya mapendekezo ya Mpango huo Februari, 2016 na kupitisha Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2016/17 – 2020/21, Aprili 2016. Nashukuru pia kwa fursa hii ya leo ya kuwasilisha hotuba yangu ya Hali ya Uchumi 2015 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17. 

3. Mheshimiwa Spika, kipekee napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wasaidizi wake wakuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu, kwa uongozi wao mahiri pamoja na juhudi za dhati wanazoweka katika kuiendeleza Tanzania ili iweze kufikia kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati mwaka 2025. 

Aidha, uongozi wao umedhihirisha dhamira ya wazi katika kupambana na ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma. Juhudi hizi zinapaswa kuungwa mkono na Waheshimiwa wabunge na Wananchi wote kwa ujumla.

4. Mheshimiwa Spika, ninaishukuru sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, chini ya Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Hawa Abdulrahaman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo kwa maoni na ushauri wao. 

Maelekezo na ushauri waliotupatia wakati wa kujadili Mapendekezo ya Mpango pamoja na maoni ya Waheshimiwa Wabunge Februari, 2016 yametusaidia katika kuandaa hotuba hii na kuboresha taarifa za Hali ya Uchumi na Mpango ninaowasilisha leo.

5. Mheshimiwa Spika, maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 yamezingatia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21). Pia, yamezingatia sera na mikakati mbalimbali ya maendeleo ya kisekta, kikanda (EAC na SADC) na Umoja wa Afrika; Malengo ya Maendeleo Endelevu, 2030; Ilani ya CCM ya Uchaguzi wa mwaka 2015; na Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kufungua Bunge la 11. 

Aidha, maandalizi hayo yamezingatia maoni ya wadau mbalimbali zikiwemo Wizara, Idara, Taasisi za Serikali, Sekta Binafsi na michango ya Waheshimiwa Wabunge waliyoitoa katika Mkutano wa Pili wa Bunge la 11.

6. Mheshimiwa Spika, mwaka 2016 ni mwaka wa kipekee kwa nchi yetu, Afrika na maendeleo ya kidunia kwa ujumla kwa sababu zifuatazo: Serikali ya Awamu ya Tano yenye kauli mbiu ya HAPA KAZI TU kuanza kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21) yenye dhima ya “kujenga Uchumi wa Viwanda na Maendeleo ya Watu” pamoja na Mpango wake wa kwanza wa maendeleo wa mwaka mmoja 2016/17; kukamilika kwa utekelezaji wa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16) uliokuwa na dhima ya kufungulia fursa za uchumi; kuanza utekelezaji wa Agenda ya Afrika 2063; na kuanza Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030. 

7. Mheshimiwa Spika, hotuba ninayowasili- sha imegawanyika katika maeneo makuu manne (4): kwanza ni maelezo kuhusu Hali ya Uchumi wa Dunia na Mwenendo wa Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2015; pili ni Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16; tatu ni Muhtasari wa Mwelekeo wa Uchumi kwa mwaka 2016/17 na nne ni Maeneo ya Kipaumbele kwa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17.

MWENENDO WA HALI YA UCHUMI 2015
Uchumi wa Dunia
8. Mheshimiwa Spika, ukuaji wa Pato la Dunia ulikuwa asilimia 3.1 mwaka 2015 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.4 mwaka 2014. Hata hivyo, mwenendo huu wa ukuaji wa uchumi unatofautiana kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea. Katika kipindi hicho, ukuaji wa uchumi kwa nchi zilizoendelea uliimarika ambapo ukuaji wa uchumi ulikuwa asilimia 1.9 mwaka 2015 ikilinganishwa na asilimia 1.8 mwaka 2014.

 Ongezeko hilo lilitokana na uwepo wa bei za chini za nishati, kuimarika kwa soko la nyumba na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha. Kwa upande wa nchi zinazoendelea, kasi ya ukuaji wa uchumi ilikuwa asilimia 4.0 mwaka 2015 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.6 mwaka 2014. Kasi ndogo ya ukuaji ilitokana na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi kwa nchi za China, Urusi, Brazil na Afrika Kusini ya Jangwa la Sahara kufuatia kuporomoka kwa bei za bidhaa/mazao katika soko la Dunia pamoja na masharti magumu ya upatikanaji wa mikopo. 

9. Mheshimiwa Spika, mwenendo wa mfumuko wa bei kwa mtumiaji wa mwisho Duniani kwa mwaka 2015 uliendelea kupungua kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta, kupungua kwa bei za bidhaa na kudhoofika kwa mahitaji ya bidhaa. Mfumuko wa bei ya mtumiaji wa mwisho Duniani ulipungua na kuwa wastani wa asilimia 3.3 mwaka 2015 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.5 mwaka 2014. Aidha, kasi ya ongezeko la bei kwa nchi zilizoendelea ilipungua kutoka wastani wa asilimia 1.4 mwaka 2014 hadi wastani wa asilimia 0.3 mwaka 2015. Hata hivyo, kasi ya mfumuko wa bei ya mtumiaji wa mwisho kwa kundi la nchi zinazoendelea iliendelea kubaki katika wastani wa asilimia 4.7 mwaka 2015 kama ilivyokuwa mwaka 2014.
Uchumi wa Taifa

Pato la Taifa na Ukuaji wa Uchumi
10. Mheshimiwa Spika, Pato halisi la Taifa lilikua kwa kiwango cha asilimia 7.0 mwaka 2015 sawa na kiwango cha ukuaji cha mwaka 2014. Ukuaji huu wa uchumi ulitokana na kuongezeka kwa ufuaji wa umeme uliosaidia katika shughuli mbalimbali ikiwemo uzalishaji viwandani; kuongezeka kwa uzalishaji wa saruji kwa ajili ya mahitaji ya shughuli za ujenzi; na kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi kwa ajili ya shughuli za kiuchumi. Katika kipindi hicho, shughuli za uchumi zilizokua kwa viwango vikubwa zilikuwa ni pamoja na: ujenzi asilimia 16.8; habari na mawasiliano (asilimia 12.1); fedha na bima (asilimia 11.8); na uchimbaji madini na mawe (asilimia 9.1). Aidha, kilimo ambacho ndio uti wa mgongo wa uchumi na kinaajiri zaidi ya asilimia 70 ya watu wote nchini kiliendelea kukua kwa kasi ndogo ya asilimia 2.3 mwaka 2015 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.4 mwaka 2014. 


Mchango katika Pato la Taifa
11. Mheshimiwa Spika, mchango wa shughuli za kilimo ambao hujumuisha mazao, ufugaji, misitu na uvuvi katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 29.0 mwaka 2015 ikilinganishwa na asilimia 28.9 mwaka 2014. 


Shughuli za viwanda na ujenzi zilikuwa na mchango wa asilimia 24.3 katika Pato la Taifa mwaka 2015 ikilinganishwa na asilimia 23.2 mwaka 2014. Vile vile, shughuli za utoaji huduma (ikijumuisha biashara na matengenezo, usafirishaji na uhifadhi mizigo, malazi, habari na mawasiliano, fedha na bima, upangishaji majumba, elimu na afya) zilikuwa na mchango wa asilimia 40.0 mwaka 2015 ikilinganishwa na asilimia 40.9 mwaka 2014. 

Pato la Wastani la kila mtu
12. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015, Tanzania ilikadiriwa kuwa na idadi ya watu 47,351,275 na Pato la Taifa lilikuwa shilingi bilioni 90,863.68. Aidha, wastani wa Pato la kila mtu lilikuwa shilingi 1,918,928 mwaka 2015 ikilinganishwa na shilingi 1,730,405 mwaka 2014, sawa na ongezeko la asilimia 10.9. Hata hivyo, Pato la wastani kwa kila mtu katika dola za Kimarekani lilipungua kutoka dola za Kimarekani 1,047 mwaka 2014 hadi dola za Kimarekani 966.5 mwaka 2015 kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania. Hivyo, ni dhahiri kuwa bado kunahitajika msukumo zaidi wa kuongeza ukuaji wa Pato la Taifa ili kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya kufikia dola za Kimarekani 3,000 kwa Pato la kila mtu na kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.


Mwenendo wa Bei
13. Mheshimiwa Spika, wastani wa mfumuko wa bei wa Taifa katika mwaka 2015 umeendelea kupungua na kubaki katika kiwango cha tarakimu moja ambapo ulipungua kufikia wastani wa asilimia 5.6 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 6.1 mwaka 2014. Kupungua kwa wastani wa kasi ya ongezeko la mfumuko wa bei nchini kulichangiwa kwa kiwango kikubwa na kushuka kwa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia na ndani na utekelezaji madhubuti wa sera za bajeti na fedha.


Jitihada za Kuondoa Umaskini
14. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2015/16, Serikali iliendelea kuratibu na kufuatilia hali ya umaskini nchini ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano na MKUKUTA-II. Matokeo ya tathmini hiyo yameainishwa katika Taarifa za Utekelezaji wa Mpango huo na MKUKUTA-II kwa kipindi cha Miaka Mitano (2010-2015). Taarifa hizo zilisambazwa kwa waheshimiwa wabunge wakati nikiwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17-2020/21) kwenye semina ya waheshimiwa wabunge Februari, 2016. Tathmini hiyo imetoa mchango mkubwa katika kubainisha vipaumbele vya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano ambao pia umejumuisha masuala ya kupambana na umaskini. 


15. Mheshimiwa Spika, kwa kutaja machache, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kukua kwa pato la wastani la mtanzania kutoka Shilingi 770,464.3 mwaka 2010 kufikia shilingi 1,918,928 mwaka 2015; kuongezeka kwa kasi ya kupungua kwa umaskini wa mahitaji ya msingi ambapo kati ya mwaka 2007 na 2012 umaskini ulipungua kwa asilimia 6.2, kutoka 34.4 hadi 28.2, ikilinganishwa na kupungua kwa kiwango cha asilimia 4.6 katika kipindi cha miaka 15, yaani kutoka asilimia 39 mwaka 1992 hadi kufikia 34.4 mwaka 2007.

16. Mheshimiwa Spika, tathmini ya hali ya umaskini kimaeneo iliyofanyika kwa kutumia takwimu za Sensa ya Watu ya mwaka 2012 na Utafiti wa Hali ya Kipato na Matumizi katika Kaya ya mwaka 2012 inaonesha matokeo chanya na kutofautiana kimkoa na kiwilaya. Mikoa 5 yenye ahueni ya umaskini wa kipato ni Dar es Salaam (asilimia 5.2), Kilimanjaro (asilimia 14.3), Arusha (asilimia 14.7), Pwani (asilimia 14.7) na Manyara (asilimia 18.3). Mikoa 5 yenye umaskini mkubwa wa kipato ni Kigoma (asilimia 48.9), Geita (asilimia 43.7), Kagera (asilimia 39.3), Singida (asilimia 38.2), na Mwanza (asilimia 35.3). Kiwilaya, umaskini mkubwa upo katika wilaya ya Kakonko (Kigoma) na Biharamulo (Kagera) ambapo takriban asilimia 60 ya watu wapo chini ya mstari wa umaskini wa mahitaji ya msingi. Hii ina maana kuwa maeneo ya vijijini hususan pembezoni bado watanzania wengi wanaishi kwenye umaskini na uwezo wao wa kupata mahitaji ya msingi ni mdogo.
Nguvu Kazi na Ajira

17. Mheshimiwa Spika, Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014 ulionesha kuwa nguvu kazi ya Taifa ilikuwa watu 25,750,116, sawa na asilimia 57 ya watu wote Tanzania Bara. Kati ya hao, wanawake walikuwa 13,390,678 (sawa na asilimia 52) na wanaume walikuwa 12,359,438 (sawa na asilimia 48). Vile vile, utafiti huo ulionesha kuwa, kati ya nguvukazi iliyokuwepo, watu wenye uwezo wa kufanya kazi walikuwa watu 22,321,924 na watu wasio na uwezo wa kufanya kazi walikuwa watu 3,428,192. Aidha, sababu za watu wasio na uwezo wa kufanya kazi zilikuwa ni pamoja na ulemavu na ugonjwa wa muda mrefu.


18. Mheshimiwa Spika, kati ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi, walioajiriwa walikuwa watu 20,030,139 na wasioajiriwa walikuwa watu 2,291,785. Kati ya walioajiriwa, wanawake walikuwa 9,886,739 (sawa na asilimia 49.4) na wanaume walikuwa 10,143,400 (sawa na asilimia 50.6). Watu wenye ajira katika jiji la Dar es Salaam walikuwa 1,927,367 sawa na asilimia 9.6 na katika maeneo mengine ya mijini walikuwa watu 5,131,422, (sawa na asilimia 25.6) na maeneo ya vijijini walikuwa watu 12,971,350, (sawa na asilimia 64.8). Kutokana na utafiti huo, ilibainika kuwa idadi kubwa ya kundi la watu walioajiriwa lilikuwa na umri kati ya miaka 35 hadi 64 (asilimia 42.5).

19. Mheshimiwa Spika, utafiti huo umeonesha vile vile kuwa, asilimia 77.8 ya nguvukazi yote ya Taifa walikuwa katika ajira. Uwiano huu wa ajira na nguvu kazi unapima uwezo wa nchi kutoa ajira. Uwiano ulikuwa mkubwa maeneo ya vijijini (asilimia 82.2), wakati jiji la Dar es Salaam lilikuwa na uwiano mdogo zaidi (asilimia 59.8). Aidha, wanaume walikuwa na uwiano mkubwa (asilimia 82.1) ukilinganisha na wanawake (asilimia 73.8). Vile vile, uwiano ulikuwa mkubwa kwa kundi la watu wenye umri wa miaka 35 - 64 (asilimia 87.2) na mdogo zaidi kwenye kundi la miaka 65 na zaidi (asilimia 56.4).
Afya

20. Mheshimiwa Spika, utafiti wa Hali ya Afya ya Mama na Mtoto uliofanyika 2015 unaonesha vifo vya watoto wachanga chini ya mwaka mmoja, vimepungua kufikia 43 mwaka 2015 kutoka 51 mwaka 2010 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai. Vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka 5 vimepungua kufikia 67 mwaka 2015 kutoka 81 mwaka 2010 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai. Upungufu wa damu kwa watoto chini ya miaka 5 umepungua toka asilimia 59 mwaka 2010 hadi 47 mwaka 2015. Viwango vya upungufu wa chakula kwa watoto chini ya miaka 5 vimepungua kutoka asilimia 8 mwaka 2010 na kufikia asilimia 34 mwaka 2015. Pia umri wa mtanzania wa kuishi umeongezeka kutoka miaka 51 mwaka 2001 hadi miaka 61 mwaka 2012.


21. Mheshimiwa Spika, utafiti huo pia unaonesha kuwa wastani wa idadi ya watoto kwa kila mama imepungua kutoka watoto 5.4 mwaka 2010 hadi 5.2 mwaka 2015. Idadi ya wasichana wanaopata watoto katika umri wa miaka 15 – 19 imeongezeka kufikia asilimia 27 mwaka 2015 kutoka asilimia 23 mwaka 2010. Kuongezeka kwa wasichana wanaoanza kupata watoto katika umri mdogo, yaani miaka 15 – 19 si dalili nzuri kwani inaashiria kuongezeka kwa utegemezi na kudumaza jitihada za kuondoa umaskini katika jamii. Ni muhimu kuongeza ushirikiano kati ya Serikali na Waheshimiwa Wabunge kuhimiza watoto wa kike kuongeza bidii katika masomo ili kwa pamoja tufanikishe jitihada za kupambana na umaskini katika maeneo ya vijijini.

22. Mheshimiwa Spika, mafanikio hayo kwa pamoja yamechangia kupandisha Kipimo cha Maendeleo ya Binadamu (Human Development Index - HDI) kutoka 0.48 mwaka 2014 hadi 0.52 mwaka 2015. Vile vile, yanaonesha kuwa, kukua kwa uchumi kumechangia kasi ya kupungua kwa umaskini wa kipato na usio wa kipato, ijapokuwa siyo kwa kasi iliyotarajiwa.

Ukuzaji Rasilimali
23. Mheshimiwa Spika, ukuzaji rasilimali uliongezeka kwa asilimia 5.4 kufikia shilingi milioni 25,328,568 mwaka 2015 kutoka shilingi milioni 24,019,720 mwaka 2014. Hata hivyo, ukuzaji rasilimali kwa bei za mwaka 2007 ulipungua kwa asilimia 1.0 na kufikia shilingi milioni 13,996,865 mwaka 2015 kutoka shilingi milioni 14,140,777 mwaka 2014. Uwiano wa ukuzaji rasilimali kwa Pato la Taifa ulikuwa asilimia 27.9 mwaka 2015 ikilinganishwa na asilimia 30.2 mwaka 2014.

Sekta ya Nje
24. Mheshimiwa Spika, mwenendo wa biashara ya bidhaa na huduma nje uliendelea kuimarika mwaka 2015 kama ilivyokuwa mwaka 2014 hususan kufuatia kupungua kwa thamani ya uagizaji wa mafuta ya petroli sambamba na kuongezeka kwa mapato ya mauzo ya bidhaa na huduma nje. Thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ilikuwa dola za Kimarekani milioni 9,450.0 ikilinganishwa na dola za Kimarekani milioni 8,717.4 mwaka 2014, sawa na ongezeko la asilimia 8.4. Ongezeko hili lilitokana na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa zisizo asilia hususan bidhaa za viwandani. Kwa upande mwingine, thamani ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ilipungua kwa asilimia 7.8 kutoka dola za Kimarekani milioni 13,586.5 mwaka 2014 hadi dola za Kimarekani milioni 12,528.2 mwaka 2015. Mwenendo huu ulichangia kuimarika kwa urari wa malipo ya kawaida.

25. Mheshimiwa Spika, urari wa biashara ya huduma ulikuwa na ziada ya dola za Kimarekani milioni 1,063.3 mwaka 2015 ikilinganishwa na ziada ya dola za Kimarekani milioni 727.3 mwaka 2014, sawa na ongezeko la ziada kwa asilimia 46.2. Ongezeko hilo lilichangiwa na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na huduma za mawasiliano, usafirishaji na usafiri hususan biashara ya utalii na kupungua kwa malipo ya huduma za usafirishaji na huduma nyingine za kibiashara.

26. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015, nchi zinazofanya biashara na Tanzania kwa kiwango kikubwa zilikuwa kama ilivyokuwa katika mwaka 2014. Nchi ambazo Tanzania iliagiza bidhaa zake kwa kiwango kikubwa zilikuwa Saudi Arabia, China, India na Umoja wa Falme za Kiarabu ambazo kwa pamoja zilichangia asilimia 55.5 ya bidhaa zote zilizoagizwa kutoka nje. Sehemu kubwa ya bidhaa zilizoagizwa na Tanzania kutoka Saudi Arabia ni bidhaa za mafuta ya petroli wakati mitambo na bidhaa za kielektroniki hususan simu za mkononi ziliagizwa kutoka China. Aidha, Tanzania iliagiza magari, makaa ya mawe, juisi na matunda kutoka India na Afrika Kusini.

27. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, nchi ambazo Tanzania iliuza bidhaa zake kwa kiwango kikubwa zilikuwa ni India, Kenya, Afrika Kusini na China ambazo kwa pamoja zilichangia asilimia 53.7 ya bidhaa zote zilizouzwa nje. Bidhaa zilizouzwa China na India ni pamoja na mbegu za mafuta, vito vya thamani, bidhaa za plastiki, dhahabu, mazao ya samaki na korosho. Kwa upande mwingine, bidhaa zilizouzwa Kenya ni chai, mahindi, maharage, vyandarua, mboga mboga na nafaka. Aidha, dhahabu, madini ya shaba, kahawa na chai ni baadhi ya bidhaa zilizouzwa Afrika Kusini.

Sekta ya Fedha
Thamani ya Fedha ya Tanzania
28. Mheshimiwa Spika, thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Kimarekani ilishuka kwa wastani wa asilimia 16.8 mwaka 2015 ikilinganishwa na asilimia 3.3 mwaka 2014. Dola moja ya Kimarekani ilinunuliwa kwa wastani wa shilingi za Tanzania 1,985.4 mwaka 2015 ikilinganishwa na shilingi 1,652.5 mwaka 2014. Kuporomoka kwa thamani ya shilingi hususan katika robo ya nne (Oktoba – Desemba 2015) ya mwaka 2015 kulitokana na sababu mbalimbali zikiwemo kuimarika kwa dola ya Kimarekani, kuchelewa kwa upatikanaji wa fedha za kigeni kwa ajili ya bajeti ya Serikali pamoja na mapato kidogo ya fedha za kigeni yasiyokidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma. Mwishoni mwa mwaka 2015, dola moja ya Kimarekani iliuzwa kwa wastani wa shilingi 2,148.5 ikilinganishwa na wastani wa shilingi 1,725.8 mwishoni mwa mwaka 2014.


Amana katika Benki za Biashara
29. Mheshimiwa Spika, amana katika benki za biashara ziliongezeka kwa asilimia 18.4 mwaka 2015 na kufikia shilingi bilioni 19,149.4 kutoka shilingi bilioni 16,177.8 mwaka 2014. Kati ya hizo, Sekta Binafsi ilichangia shilingi bilioni 18,292.5 ambazo ni sawa na asilimia 95.5 ya amana zote. Amana za fedha za kigeni na amana za akiba na za muda maalum zilichangia sehemu kubwa ya amana zote kwenye benki za biashara mwaka 2015. Uwiano wa amana za fedha za kigeni katika amana zote uliongezeka na kufikia asilimia 32.9 mwaka 2015 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 28.8 mwaka 2014. Aidha, uwiano wa amana za akiba na za muda maalum ulikuwa wastani wa asilimia 32.4 mwaka 2015.


Mikopo ya Benki za Biashara kwa Shughuli za Kiuchumi
30. Mheshimiwa Spika, mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa asilimia 24.8 mwaka 2015 zaidi ya lengo la asilimia 24.0 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 19.4 mwaka 2014. Hii ilitokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kupungua kwa ukuaji wa madai rasmi kwa Serikali. Madai rasmi kwa Serikali Kuu yalikua kwa asilimia 33.8 mwaka 2015 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 42.9 mwaka 2014. Aidha, thamani ya mikopo iliyotolewa kwa sekta binafsi ilikuwa sawa na asilimia 17.3 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 15.6 katika mwaka 2014. Ukuaji wa mikopo kwenye shughuli za uchukuzi na mawasiliano; mikopo kwa watu binafsi; na kwenye shughuli za viwandani uliongezeka mwaka 2015 ikilinganishwa na mwaka 2014. Katika kipindi hicho, sehemu kubwa ya mikopo ilielekezwa katika shughuli za biashara ambazo zilipata wastani wa asilimia 20.2 ya mikopo yote ikifuatiwa na shughuli za watu binafsi (asilimia 18.0).


Mwenendo wa Viwango vya Riba
31. Mheshimiwa Spika, viwango vya riba za amana na za mikopo viliongezeka mwaka 2015 ikilinganishwa na viwango vya mwaka 2014. Riba ya mikopo kwa ujumla iliongezeka kutoka wastani wa asilimia 15.75 Desemba 2014 hadi wastani wa asilimia 16.41 Desemba 2015. Riba za amana za muda maalum ziliongezeka kutoka wastani wa asilimia 8.76 Desemba 2014 hadi wastani wa asilimia 9.22 Desemba 2015.


32. Mheshimiwa Spika, kiwango cha riba za amana za mwaka mmoja kiliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 11.08 Desemba 2015 kutoka wastani wa asilimia 10.66 Desemba 2014. Hata hivyo, riba ya mikopo ya mwaka mmoja ilipungua kutoka wastani wa asilimia 14.80 Desemba 2014 hadi wastani wa asilimia 14.22 Desemba 2015. Kutokana na mwenendo huu, tofauti kati ya riba za amana na za mikopo za mwaka mmoja ilipungua kutoka wastani wa asilimia 4.14 Desemba 2014 hadi wastani wa asilimia 3.14 Desemba 2015. Kwa upande mwingine, riba katika soko la fedha baina ya mabenki zilipungua na kuwa wastani wa asilimia 7.29 Desemba 2015 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 11.82 Desemba 2014.

33. Mheshimiwa Spika, riba kwenye dhamana za Serikali zilikuwa wastani wa asilimia 18.25 mwaka 2015 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 15.73 mwaka 2014. Aidha, mauzo ya dhamana za Serikali yalipungua kwa asilimia 8.5 kutoka mauzo yenye thamani ya shilingi bilioni 3,535.7 mwaka 2014 hadi shilingi bilioni 3,235.3 mwaka 2015. Mauzo ya hatifungani kwa mwaka 2015 yaliongezeka na kufikia shilingi bilioni 924.6 kutoka shilingi bilioni 916.7 mwaka 2014, sawa na ongezeko la asilimia 0.9. 

Mapato na Matumizi ya Serikali
34. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/16, Serikali ilipanga kukusanya jumla ya shilingi bilioni 22,495.5 kutoka kwenye vyanzo vya ndani na nje. Sera za mapato ya ndani katika mwaka 2015/16 zililenga kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya shilingi bilioni 13,475.6 sawa na asilimia 14.3 ya Pato la Taifa. Katika kipindi cha Julai 2015 hadi Aprili 2016, makusanyo ya ndani (ikijumuisha ya Halmashauri) yalikuwa shilingi bilioni 11,481.4 sawa na asilimia 99 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 11,550.8 katika kipindi hicho. Mapato ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 10,170.1 sawa na asilimia 100 ya lengo na mapato yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 967.2 sawa na asilimia 105 ya lengo. Vile vile, mapato ya Halmashauri yalikuwa shilingi bilioni 344.1 sawa na asilimia 79 ya lengo kwa kipindi hicho.


35. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/16, Serikali ilikadiria kutumia jumla ya shilingi bilioni 22,495.5 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo. Kiasi hiki kinajumuisha shilingi bilioni 16,576.4 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 5,909.1 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Katika kipindi cha Julai 2015 hadi Aprili 2016, Serikali ilitumia jumla ya shilingi bilioni 16,856.9 sawa na asilimia 90 ya lengo katika kipindi hicho. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 13,647.1 zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 3,209.8 zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. 


Uendelezaji wa Sekta Binafsi
Uwekezaji Vitega Uchumi Nchini
36. Mheshimiwa Spika, uwekezaji wa moja kwa moja nchini kutoka nje umeendelea kuongezeka ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, thamani ya uwekezaji wa moja kwa moja nchini iliongezeka kutoka dola za Kimarekani milioni 1,229 mwaka 2011 hadi dola za Kimarekani milioni 2,142 mwaka 2014. Ongezeko hilo limetokana na kuimarika kwa mazingira ya kufanya biashara nchini pamoja na sera na sheria imara za kuvutia uwekezaji nchini.


Urahisi wa Kufanya Biashara Nchini
37. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Urahisi wa Kufanya Biashara ya Benki ya Dunia ya mwaka 2015, Tanzania ilipanda kwa nafasi moja katika vigezo vya urahisi wa kufanya biashara kwa kushika nafasi ya 139 kati ya nchi 189 Duniani ikilinganishwa na nafasi ya 140 mwaka 2014. Mafanikio hayo kidogo yalitokana na kuboreshwa kwa taratibu za upatikanaji wa vibali vya ujenzi na huduma za biashara kupitia vituo vya pamoja vya utoaji huduma mipakani.


38. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina ya Hali ya Uchumi wa Taifa yapo katika kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015.

UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2015/16
Utekelezaji wa bajeti ya Maendeleo 2015/16
39. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/16, Serikali ilitenga shilingi bilioni 5,909.1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, fedha za ndani ni shilingi bilioni 4,246.9 na fedha za nje ni shilingi bilioni 1,662.2. Fedha zilizotengwa kwa ajili ya Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri ni shilingi bilioni 739.4 ambapo fedha za ndani ni shilingi bilioni 595.0 na fedha za nje ni shilingi bilioni 144.4. Kwa upande wa Wizara, Taasisi, Wakala na Idara zinazojitegemea zilitengewa shilingi bilioni 5,169.7 ambapo fedha za ndani ni shilingi bilioni 3,651.9 na fedha za nje ni shilingi bilioni 1,517.8.


40. Mheshimiwa Spika, fedha za miradi ya maendeleo zilizotolewa hadi Aprili 2016 ni shilingi bilioni 3,209.8. Kati ya fedha hizo, fedha za ndani ni shilingi bilioni 2,819.9 na fedha za nje ni shilingi bilioni 398.841. Fedha hizo za maendeleo zilizotolewa ni sawa na asilimia 65 ya lengo la shilingi bilioni 4,922.5 hadi Aprili 2016. Fedha za ndani zilizotolewa ni sawa na asilimia 79 ya lengo la shilingi bilioni 3,537.4 na fedha za nje zilizotolewa ni sawa na asilimia 29 ya lengo la shilingi bilioni 1,385.2.

Miradi iliyokamilika mwaka 2015/16
41. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa taarifa za mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na changamoto zake zilishaelezwa kwa kina katika hotuba za kisekta zilizotangulia, naomba sasa nitaje baadhi ya miradi ya maendeleo iliyokamilika kama kielelezo cha mafanikio yaliyopatikana katika mwaka 2015/16:-
(i) Ujenzi wa madaraja ya Kigamboni, Maligisu, Nangoo, Mbutu na Ruhekei katika barabara kuu;
(ii) Ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam (km 542);
(iii) Ujenzi wa mitambo ya kuchakata gesi katika maeneo ya Madimba na Songosongo;
(iv) Ujenzi wa vituo vya kupokelea gesi vya Somanga – Fungu na Kinyerezi;
(v) Usimikaji wa mitambo minne ya kufua umeme Kinyerezi I yenye uwezo wa kuzalisha MW 150 na kuanza uzalishaji wa umeme;
(vi) Awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini (REA Turnkey Phase II) na hivyo kuunganisha wateja 61,023 wa awali kati ya wateja 250,000;
(vii) Kukamilika kwa awamu ya Pili ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (km 25,954) na kusambazwa katika mikoa 24 Tanzania Bara;
(viii) Kukamilika kwa mradi wa Maji wa Ruvu Chini (Pwani); na
(ix) Kukamilika kwa miradi mipya 1,160 ya maji ya vijiji 10 katika vijiji 1,206 yenye vituo 28,499 vya kuchotea maji katika Halmashauri 148. 


42. Mheshimiwa Spika, miradi mingine katika maeneo ya kipaumbele (miundombinu, kilimo, viwanda, maendeleo ya rasilimali watu; utalii, huduma za kifedha na Biashara) ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. 

43. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo yapo katika Kitabu cha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 (Sura ya Pili).

Changamoto na Hatua zilizochukuliwa
44. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/16, kumejitokeza changamoto mbalimbali katika kutekeleza Mpango ikiwa ni pamoja na: upatikanaji wa fedha za kugharamia miradi; ulipaji fidia kwa wakati; taratibu na gharama za ununuzi wa umma; madeni ya wakandarasi, hususan ya ujenzi wa barabara; upatikanaji wa ardhi ya uwekezaji; utegemezi wa bajeti ya maendeleo; ushiriki mdogo wa sekta binafsi; mazingira yasiyo wezeshi kwa uwekezaji na uendeshaji biashara; na uhaba wa miundombinu wezeshi (barabara, maji na umeme) ya kuwezesha utekelezaji wa miradi.


45. Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto hizo ikiwemo:- kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali fedha, hususan fedha za miradi ya Matokeo Makubwa Sasa na miradi ya Kitaifa ya Kimkakati; kuboresha mazingira ya uendeshaji biashara ili kuchochea uwekezaji wa Sekta Binafsi, hususan wa viwanda; kuendelea kuimarisha miundombinu wezeshi katika maeneo ya miradi ya maendeleo; na kupunguza madeni.

Hali ya Viwanda Nchini
46. Mheshimiwa Spika, mchango wa sekta ya uzalishaji viwandani katika Pato la Taifa kwa kipindi cha mwongo mmoja uliopita ni wastani wa asilimia 7 ambapo uliongezeka kutoka asilimia 6.6 mwaka 2005 hadi asilimia 7.3 mwaka 2015. Kwa mujibu wa sensa ya viwanda ya mwaka 2013, Tanzania ina jumla ya viwanda 50,656 ambavyo vipo katika mikoa mbalimbali nchini. Viwanda hivyo vinajumuisha viwanda vya kati na vikubwa 1,769 sawa na asilimia 3.5 ambavyo vinaajiri wafanyakazi 10 na kuendelea, na viwanda vidogo 48,887 sawa na asilimia 96.5 ambavyo vinaajiri wafanyakazi 1 hadi 9. Takriban ajira 231,176 zimetengenezwa kutokana na viwanda hapa nchini, ambapo viwanda vikubwa na vya kati vimetoa ajira 107,732 na viwanda vidogo ajira 123,364. 


47. Mheshimiwa Spika, mikoa inayoongoza kwa idadi kubwa ya viwanda ni Dar es Salaam 516 (asilimia 29.2), Arusha 144 (asilimia 8.1), Shinyanga 101 (asilimia 5.7), Kilimanjaro 96 (asilimia 5.4) na Mwanza 88 (asilimia 5.0). Vilevile, aina ya viwanda vingi vilivyopo nchini ni vya uzalishaji wa vyakula 20,228 (asilimia 39.9), mavazi (kanga na vitenge) 13,758 (asilimia 27.2) na samani 7,071 (asilimia 14.0). Hata hivyo, zipo fursa zaidi katika viwanda vingine ambavyo utafiti ulionesha viwanda vyake vipo vichache nchini kama vile nguo 817, TEHAMA 3, mashine na vifaa 30, madawa 9, ngozi 216, kemikali 102 na vifaa vya umeme 269.

Ubinafsishwaji wa Viwanda
48. Mheshimiwa Spika, katika kukidhi mahitaji ya soko huria na ushindani wa kibiashara viwanda 106 vilibinafsishwa kwa lengo la kuongeza ufanisi, uzalishaji, ajira, kupunguza uagizaji wa bidhaa nchini na kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi. Kati ya viwanda vilivyobinafsishwa, uzalishaji katika viwanda 34 umekuwa wa ufanisi na hivyo kuongeza ajira na mapato ya kodi kwa Serikali. Aidha, viwanda 33 vinaendeshwa kwa hasara na viwanda 39 vilivyokuwa vinazalisha bidhaa mbalimbali kama vile ngozi, chuma, korosho, zana za kilimo, sabuni na mafuta ya kupikia vimefungwa kabisa. Changamoto kubwa zinazovikabili viwanda vilivyobinafsishwa ni pamoja na mtaji, teknolojia, malighafi na upatikanaji wa umeme wa uhakika, maji na masoko. Aidha, baadhi ya viwanda vilivyobinafsishwa vilitumika kama dhamana ya kupata mikopo ya benki, na kugharamia shughuli nyingine badala ya uendelezaji viwanda na hivyo kuwa na madeni.


Mikakati ya Kuendeleza Viwanda Nchini
49. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza kwa vitendo dhima ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, Mpango huu pamoja na mambo mengine utajikita katika kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuendeleza viwanda vikubwa, vya kati, vidogo na vile vilivyobinafsishwa.


50. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kulipa fidia kwa maeneo maalum ya uwekezaji na kuweka miundombinu wezeshi itakayovutia Sekta Binafsi kuwekeza katika viwanda vikubwa; kuendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini ili kuinua nafasi ya Tanzania katika ushindani wa kibiashara; kuendelea kuboresha miundombinu ya msingi kuwezesha maendeleo ya viwanda nchini hususan, miradi ya nishati ya umeme, maji, barabara, reli na bandari; na kuboresha sekta ya fedha ili iweze kutoa mitaji ya kuendeleza viwanda. 

51. Mheshimiwa Spika, Mikakati mingine ni pamoja na: kusimamia kikamilifu uingizwaji wa bidhaa zinazozalishwa na viwanda hapa nchini; kuendeleza miundombinu ya SIDO ili kuvutia viwanda vidogo; kuweka mikakati madhubuti ya kuwainua wajasiriamali wadogo na wa kati ili waweze kuzalisha kwa ufanisi; kuboresha mazingira ya biashara nchini ikiwa ni pamoja na kufuta kodi na tozo ambazo ni vikwazo kwa wajasiriamali wadogo; kuanzisha kongane za viwanda (Industrial Clusters) za kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu; na kuhamasisha ushiriki wa Sekta Binafsi kupitia elimu na mafunzo ya kuendesha na kuendeleza viwanda, ujasiriamali na uwekezaji.

52. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutathmini kwa kina viwanda vyote vilivyobinafsishwa ili kuandaa mikakati ya kuviendeleza; kupitia mikataba yote ya ubinafsishaji na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria; kufufua viwanda vilivyobinafsishwa na kuviendeleza kwa utaratibu wa Ubia kati ya sekta ya umma na Sekta Binafsi; na kuchukua hatua kuhusu uagizwaji wa bidhaa zinazozalishwa na viwanda hapa nchini ili viweze kukua zaidi.

53. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu Hali ya Viwanda nchini yapo katika kitabu cha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 (Sura ya Tatu).

MWELEKO WA UCHUMI 2016
54. Katika mwaka 2016/17, shabaha na malengo ya uchumi jumla na bajeti ni kama ifuatavyo:-
(i) Pato Halisi la Taifa kukua kwa asilimia 7.2 mwaka 2016 kutoka 7.0 mwaka 2015;
(ii) Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja kati ya asilimia 5.0 na asilimia 8.0 mwaka 2016;
(iii) Mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri kufikia asilimia 14.8 ya Pato la Taifa mwaka 2015/16, na kuendelea kuongezeka kufikia asilimia 16.9 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17;
(iv) Mapato ya kodi kufikia asilimia 13.8 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17 kutoka asilimia 12.6 ya Pato la Taifa mwaka 2015/16;
(v) Matumizi ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 23.2 ya Pato la Taifa mwaka 2015/16 hadi asilimia 27.0 mwaka 2016/17;
(vi) Nakisi ya bajeti inakadiriwa kuwa asilimia 4.5 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17 kutoka makadirio ya bajeti ya asilimia 4.2 mwaka 2015/16;
(vii) Nakisi katika urari wa malipo ya kawaida kuwa asilimia 7.9 ya Pato la Taifa mwaka 2015/16 na kupungua hadi asilimia 7.5 mwaka 2016/17; na
(viii) Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne ifikapo Juni 2017.


MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA 2016/17
Maeneo ya Kipaumbele 2016/17
55. Mheshimiwa Spika, Miradi ya maendeleo ya kipaumbele katika mwaka 2016/17 imegawanyika katika makundi manne (4) yafuatayo: Viwanda vya Kukuza Uchumi na Ujenzi wa Msingi wa Uchumi wa Viwanda; Kufungamanisha Maendeleo ya Uchumi na Rasilimali Watu; Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara na Uwekezaji; na Usimamizi wa Utekelezaji wa Mpango.


56. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Viwanda vya Kukuza Uchumi na Ujenzi wa Msingi wa Uchumi wa Viwanda miradi itakayotekelezwa ni pamoja na: mradi wa Magadi Soda – Bonde la Engaruka, Arusha; mradi wa kufufua Kiwanda cha General Tyre, Arusha; uendelezaji wa viwanda vidogo – SIDO katika maeneo ya viwanda (Industrial Park) ya Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya na Morogoro.

57. Mheshimiwa Spika, miradi itakayotekelezwa katika eneo la Kufungamanisha Maendeleo ya Uchumi na Rasilimali Watu ni pamoja na: Kuimarisha mifumo, majengo na miundombinu mingine katika shule za awali, msingi na sekondari; upanuzi na ujenzi wa vyuo vikuu; ukarabati, upanuzi na ujenzi wa vyuo vya ualimu; na ukarabati, upanuzi na ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi; mradi wa kuboresha hospitali za rufaa; Taasisi ya Saratani Ocean Road; na hospitali ya magonjwa ya kuambukiza Kibong’oto; na kuanzisha Progamu ya kuzalisha Ajira na Programu ya Maendeleo ya Ujuzi; Mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.

58. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara na Uwekezaji, Serikali itaendelea kutekeleza miradi iliyoanza kutekelezwa katika kipindi cha Mpango wa kwanza wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16), ikiwa ni pamoja na miradi katika maeneo yafuatayo: nishati (ikiwemo mradi wa Liquified Natural Gas); kilimo cha mazao; mifugo; uvuvi; misitu; maji; miundombinu ya reli na barabara hususan: Kidahwe – Nyakanazi, Masasi – Newala - Mtwara, Mbinga - Mbamba Bay na Tabora – Ipole – Koga - Mpanda; bandari hususan ya Dar es Salaam, Bagamoyo na Mtwara; usafiri wa anga; usafiri wa majini na TEHAMA.

59. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17, Serikali itaimarisha Usimamizi wa Utekelezaji wa Mpango kwa lengo la kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika utekelezaji wa mipango na programu mbalimbali za maendeleo. Dhamira ya Serikali ni kuongeza kasi katika kutanzua vikwazo vya utekelezaji na kuimarisha usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya Mpango kwa kurekebisha taratibu zitakazosaidia na kuongeza ufanisi wa utekelezaji.

60. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 umeainisha Miradi Mikubwa ya Kielelezo ambayo itapewa msisitizo katika utekelezaji wake. Miradi hii ni mahsusi kwa maana ya ukubwa wa uwekezaji na matokeo tarajiwa. Miradi hiyo ni pamoja na: mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma; mradi wa chuma Liganga; ujenzi wa reli mpya ya Kati Dar – Kigoma na Tabora – Mwanza na matawi yake Isaka – Kigali/Keza – Musongati na Kaliua - Mpanda kwa kiwango cha standard gauge; uboreshaji wa usafiri katika maziwa makuu ikiwa ni pamoja na ununuzi wa meli moja mpya ya usafirishaji wa abiria na mizigo katika Ziwa Victoria na ukarabati wa meli za MV Victoria, MV Butiama na MV Liemba na kuimarisha Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) ikijumuisha ununuzi wa ndege tatu (3) mpya moja (1) ikiwa ni Bombardier CS300 yenye uwezo wa kubeba abiria 100 – 150 na ndege mbili (2) Bombardier Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 67 – 88 kila moja.

Mikakati ya Kushirikisha Sekta Binafsi 2016/17
61. Mheshimiwa Spika, Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 utategemea zaidi ushiriki mkubwa wa Sekta Binafsi. Hivyo, Serikali imeweka mikakati ya kujenga na kuboresha miundombinu wezeshi, kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara, kuhamasisha ubia kati ya Sekta Binafsi na sekta ya umma. Jitihada mahsusi za Serikali katika eneo hili ni pamoja na: kuongeza kasi ya kulipa fidia katika Maeneo Maalum ya Uwekezaji (EPZs na SEZs); Benki ya Rasilimali Tanzania kuongeza utoaji wa mikopo katika sekta mbalimbali kutoka shilingi bilioni 538.7 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 726.9 mwaka 2016; kuitangaza Benki ya Maendeleo ya Kilimo na huduma zake ili wananchi waweze kutumia fursa za mikopo zinazopatikana katika benki hiyo na kuwezesha Kituo cha Uwekezaji Tanzania kuwa na ardhi yenye hati miliki kwa ajili ya kuikodisha kwa wawekezaji wa nje.


62. Mheshimiwa Spika, Mpango huu utahusisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kwa njia ya ubia ili kuendelea kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi. Miongoni mwa miradi itakayotekelezwa kwa ubia ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Biashara na Huduma Kurasini, miradi ya Chuma - Liganga na makaa ya mawe - Mchuchuma; na mradi wa barabara wa Dar es Salaam – Chalinze – Morogoro Express Way.
63. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu Miradi ya Kipaumbele yapo katika kitabu cha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 (Sura ya Nne).

Ugharamiaji wa Mpango 2016/17
64. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17 Serikali imetenga shilingi bilioni 11,820.503 sawa na asilimia 40 ya bajeti yote ili kutekeleza miradi ya maendeleo. Aidha, fedha za ndani ni shilingi bilioni 8,702.697 sawa na asilimia 74 ya bajeti ya maendeleo na fedha za nje shilingi bilioni 3,117.805 sawa na asilimia 26 ya bajeti ya maendeleo. Sekta binafsi inatarajiwa kuwekeza kiwango kikubwa cha fedha ili kuanzisha na kuendeleza viwanda ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango. Kwa ujumla fedha za maendeleo zimeelekezwa zaidi katika miradi inayolenga kuendeleza viwanda kama vile uchukuzi, ujenzi, nishati, kilimo, maji, elimu na afya.

65. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu Ugharamiaji wa Mpango yapo katika kitabu cha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 (Sura ya Tano).

Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji wa Taarifa
66. Mheshimiwa Spika, Wizara na Taasisi za umma zinahusika moja kwa moja katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo katika maeneo yao na kuandaa taarifa za utekelezaji za kila robo mwaka na mwaka mzima. Taarifa za ufuatiliaji na tathmini za miradi ya maendeleo zitawasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango. Aidha, Ofisi ya Rais – TAMISEMI itaratibu ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo itakayotekelezwa katika ngazi za Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Wizara na Taasisi zitakuwa na jukumu la kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi ya Kitaifa ya Kimkakati na ya Sekta Binafsi kwa lengo la kubaini changamoto zinazokabili miradi hiyo na kuzitafutia ufumbuzi.


67. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji taarifa yapo katika kitabu cha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 (Sura ya Sita).

SHUKRANI
68. Mheshimiwa Spika, kabla ya kumaliza hotuba yangu napenda kumshukuru Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Dr. Ashatu Kijaji (Mb), Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara zote, Wakuu wa Idara za Serikali na Taasisi zinazojitegemea kwa ushirikiano wao wakati wote wa maandalizi ya kutayarisha Taarifa ya Hali ya Uchumi 2015 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/17. Vile vile, napenda kuwashukuru watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu Dkt. Servacius B. Likwelile kwa kusimamia vizuri kazi za kila siku na maandalizi ya Taarifa ya Hali ya Uchumi 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 na hotuba hii.

69. Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana katika hali ya uchumi na utekelezaji wa Mpango yamechangiwa na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wakiwemo nchi marafiki, washirika wa maendeleo, sekta binafsi na wananchi wote. Kwa niaba ya Serikali, ninawashukuru wadau hao kwa michango yao.

HITIMISHO
70. Mheshimiwa Spika, hotuba hii na vitabu vya Taarifa ya Hali ya uchumi 2015, na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 vinapatikana katika tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango www.mof.go.tz na www.mipango. go.tz

71. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa Waheshimiwa Wabunge wapokee, kujadili na kupitisha Taarifa ya Hali ya Uchumi 2015 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17.

72. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata