CHADEMA YAONDOA KESI YAKE MAHAKAMANI DHIDI YA JESHI LA POLISI.

Chadema imeondoa mahakamani kesi dhidi ya polisi ya kupinga amri ya kupiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara, baada ya kubainika mapungufu ya kisheria katika hati yao ya mashtaka. 

Akizungumza na mwandishi wa habari hii ofisini kwake jana, Jaji Mohamed Gwae aliyepangwa kusikiliza shauri hilo alitaja mapungufu ya kisheria yaliyobainika kwenye hati ya mashtaka ya Chadema kuwa ni pamoja na kumjumuisha katika hati ya mashtaka Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Mssanzya, ambaye kisheria alistahili kufunguliwa shtaka katika masjala kuu (main registry). 

“Baada ya kushauriana na mawakili wa Chadema kuhusu suala hilo, waliamua kwa hiari yao kuondoa kesi yao kwa ajili ya kuifanyia marekebisho hati yao ya mashtaka,” alisema Jaji Gwae.

Akifafanua, Jaji huyo alisema Chadema wana njia mbili za kurekebisha kasoro hiyo; moja ni kufungua shauri hilo masjala kuu ya mahakama jijini Dar es Salaam ili kuendelea kumshtaki Kamishina Mssanzya. 

Njia ya pili kwa mujibu wa Jaji Gwae ni Chadema kuendelea na shauri hilo jijini Mwanza dhidi ya wakuu wa polisi wa wilaya za Maswa, Kahama na Geita bila kumjumlisha Kamishna Mssanzya. 

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutoka ofisini kwa Jaji, Wakili wa Chadema, John Mallya aliyekuwa na mwenzake Paul Kipeja, alisema shauri hilo halikuanza kusikilizwa jana kutokana na kutokamilika kwa taratibu za kiofisi za kimahakama.

"Shauri letu bado lipo na tayari limepangiwa Jaji wa kuisikiliza; ni imani yangu kuwa kesho (leo), hatima ya kesi yetu itajulikana,” alisema kwa kifupi wakili Mallya bila kutoa maelezo zaidi. 

Juni 10, mwaka huu, Chadema ilifungua kesi mahakamani kupinga amri ya polisi ya kupiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara ya kisiasa, kwa kile kilichodaiwa kuwa ni tishio la kiusalama. 

Katika hati ya mashtaka iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, Chadema inaiomba mahakama kutamka kuwa amri hiyo ni batili na utekelezaji wake pia ni batili. 

Maombi mengine ni mahakama kutoa zuio la kimahakama kwa polisi kutotoa amri za aina hiyo tena na mahakama kuruhusu vyama vya siasa kuendelea na shughuli za kisiasa, ikiwamo maandamano na mikutano ya hadhara, huku polisi wakiagizwa kulinda usalama kama sheria inavyoagiza.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata