BARUA YA WAZI: TUNAVAA YEBOYEBO WAO WANAPIGA MARUFUKU PLASTIKI

NA GORDON KALULUNGA
KATIKA nchi hii tuna vitu vingi vizuri, lakini vipaumbele vyetu vina hila ndani yake. Jambo hili linatimilika kutoka katika maandiko ya Biblia yasemayo “Mna hila nyingi moyoni mwa mtu, lakini shauri la Bwana ndilo litakalosimama” Mithali 19;21.

Hatuna shule za uhakika, hatuna hospitali za uhakika, hatuna dawa za kutibu binadamu za uhakika, hatuna uzazi wa mpango wa uhakika, hatuna barabara za uhakika, hatuna reli za uhakika, hatuna viwanda vya uhakika, hatuna ahadi za uhakia na wala hatuna sera na sheria zinazotekelezwa kwa uhakika.

Tulipofikia ni kwamba tuna vitu vikuu sita ambavyo tuna uhakika navyo, vitu hivyo ni ugeugeu wa uhakika, porojo za uhakika, uvivu wa uhakika, fitina za uhakika, rushwa za uhakika na usahaulifu wa uhakika . Ni tatizo lililo ndani yetu kama taifa.

Serikali imeendelea kupiga marufuku mambo kadhaa hapa nchini bila kujiandaa na matokeo yake watu wakisema wanaonekana kama wachochezi na hawaitakii mema serikali iliyopo madarakani jambo ambalo si sawa na baadhi waliomo ndani ya chama tawala kuanza kusemana vibaya kuwa ni mamluki!

Tumeshuhudia marufuku ya sukari kutoka nchi za nje na adha yake kwawatanzania hasa masikini. Lakini hivi karibuni serikali imeendelea kutoa matamko mazito kwa watu wa nyikani likikiwemo suala la kupiga marufuku mifuko ya Naironi (Plastic).

Katika jambo hili sioni kama serikali na watoa matamko kama wana
makosa, bali naona wamepatia kabisa kwasababu wameanza kujipambanuawazi kuwa wao hawatokani miongozi mwetu. Hawayajui mahitaji yetu halisi. Masikini na wao wapo mbali sawa na mbingu na ardhi. 

Bali kipindi cha kampeni ndipo wanakuwa pamoja nao na wapiga kurawanachukua rushwa kwasababu hawawaamini kama wataweza kurudimajimboni.

Lakini serikali inapaswa kujihoji kabla ya matamko yake ambapo kwa leo nitatoa mifano michche sana hasa katika marufuku ya Serikali kuwa ni marufuku watanzania kutumia mifuko ya plastiki kwa madai kuwa inaharibu mazingira.

Athari hizo ni kweli kabisa zipo wazi na hakika kwa utii wa Watanzania naamini serikali ikiamua kuwakomesha wakaidi watakoma.

Tujiulize kidogo kuwa, serikali hii ya awamu ya tano kila uchwapo
inahubiri kufufua na kujenga viwanda vipya nchini kwa lengo la kufikia ahadi kwa watanzania kuwa wananchi wanapaswa kuwa na uchumi wa kati na hiyo ni kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 na mwelekeo wa chama hicho wa mwaka 2010-2025.

Je viwanda hivyo vitakuwa viwanda vya namna gani na usindikaji wa bidhaa zitakazokuwa zinazalishwa zitawekwa kwenye nini? Pale mkoani Tanga kuna kiwanda kinaitwa Amboni Plastic, kinazalisha bidhaa ambazo haziozi je kitafungwa baada ya amri hii ya serikali?

Viwanda vya vinywaji je vitafungwa? Maana tumeshuhudia vinywaji vingi kwa sasa vinasindikwa na kuuzwa katika chupa za plastiki ambazo chupa hizo haziozi.

Magunia tuliyokuwa tunayatumia kutokana na uzalishwaji uliokuwa
unatokana na katani sasa hayapo na hayapatikana  kirahisi.

Wanaopata ni matajiri maana yamekuwa ni mifuko ya kitalii na wanamudu matajiri ambao miongoni mwao ni hawa wanaopiga marufuku bidhaa ambazo masikini wapiga kura wanazimudu.

Huku kwetu Nyikani viatu vyetu vya kutegemewa mashuleni, kwenye nyumba za ibada, harusini, majumbani na hata michezoni ni viatu vya plastiki maarifu kama Yeboyebo. Je serikali inalijua jambo hili? Bei ya viatu vyetu hivi serikali inazijua na kwamba siyo kuwa tunafanmya makusudi bali tunalazimika kutokana na uchumi wetu ambao haumudu kugharamia ununuzi wa viatu vya ngozi?

Ninaamini kuwa kila mamlaka iliyopo duniani inatoka kwa Mungu na ndiyo maana Rais Dkt. John Magufuli hivi karibunbi alitamka wazi kuwa urais wake hakupewa na mtu bali alipewa na Mungu.

Tutaendelee kutii lakini hatutaacha kusema ukweli hata kama tunajua kuwa mkweli ni hatari zaidi kuliko kuwa muongo na mpaka mafuta wakubwa kwa mgongo wa chupa.

Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki ardhi ya Magufuli na kuwasamehe wenye maamuzi pale wanapowakosea wapiga kura kwa kujua ama kutokujua kutokana na maamuzi yao.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata