SIRI YA MAALIM SEIF KUKAA SERENA HOTEL NA GHARAMA ALIZOTUMIA ZAANIKWA.

SIRI imefichuka kuhusu hatua ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK), Maalim Seif Sharif Hamad, kuishi hotelini jijini Dar es Salaam.

Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), amekuwa akiishi katika Hoteli ya Serena jijini Dar tangu aliporuhusiwa kutoka Hospitali ya Hindu Mandal Machi 8, mwaka huu alipokuwa amelazwa kwa matibabu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, mmoja wa ofisa wa ngazi za juu wa CUF, alishangazwa na hatua ya baadhi ya watu kuhoji kiongozi huyo kuendelea kuishi hotelini hapo.

Alisema hatua ya kiongozi huyo kuishi hotelini ni matokeo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kushindwa kutekeleza ahadi ya kumpa nyumba pindi anapokuwa Dar es Salaam katika shughuli zake.

Alisema kutokana na hali hiyo imekuwa ni utaratibu kwa kiongozi huyo kufikia katika hoteli hiyo na gharama za kuishi hotelini hapo hulipwa na SMZ kwa mujibu wa sheria.

“Tangu mwaka 2010 Maalim aliahidiwa atapewa nyumba na Serikali ya SMZ lakini hilo halijafanyika, hiyo nyumba hajapewa hadi leo ndiyo maana mara zote akija Dar hufikia hotelini.

“SMZ ndiyo wenye jukumu la kulipa na si vinginevyo, kwani hata kama kama kuna viongozi wa SMZ wamepewa nyumba kwa muda wote, lakini Maalim Seif hajapewa, sasa kama unataka kujua kwa undani unaweza kuwauliza viongozi wa Serikali wao ndiyo wenye majibu zaidi,” alisema ofisa huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe

Gharama zilizotumika kwa siku 7
Kwa mujibu wa chumba anachoishi kiongozi huyo chenye hadhi ya rais ambacho hutozwa kwa Dola za Marekani 2,801.50, ambapo dola moja ni sawa na Sh 2,180. Hivyo kwa siku saba hadi kufikia leo Serikali imemlipia Maalim Seif,  Sh milioni 42.946.

Kauli ya CUF
Alipotafutwa Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Hamad Masoud Hamad, alisema hatua ya Maalim Seif kuishi hotelini inatokana na maagizo ya daktari wake ambaye amemtaka apumzike kwa sasa.

Alisema kutokana na hali hiyo baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali alipokuwa akipatiwa matibabu alikwenda katika Hoteli ya Serena anapofikia kila mara anapokuwa jijini Dar es Salaam.

Alipoulizwa ni nani anayelipa gharama za kuishi hotelini hapo, Hamad alisema wanaoweza kuzungumzia suala hilo ni viongozi wa SMZ.

“Magufuli (Rais), alipokwenda kumwona alimuuliza ni nani anayemlipia gharama za hoteli na Maalim alisema wazi ni SMZ, lakini ninachotaka kuwaambia Maalim Seif hana nyumba Dar es Salaam.

“… kama wapo viongozi waliopewa nyumba wa SMZ ni hao lakini si Maalim Seif, tangu mwaka 2010 hana nyumba na hufikia hotelini, hana nyumba ya Serikali wala yake binafsi,” alisema Hamad.

SMZ wazungumza
Alipotafutwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, alisema Maalim Seif anastahiki zake kama kiongozi wa SMZ ikiwemo kupatiwa haki ya matibabu pamoja na mahala pa kuishi.

“SMZ ni wajibu wake kuwahudumia viongozi na wananchi wake kwa ujumla, Maalim Seif bado ni Makamu wa Kwanza wa Rais hivyo ana wajibu wa kuhudumiwa.

“Na katika hili anahudumiwa na SMZ ikiwemo kulipiwa hoteli pindi awapo nje ya Zanzibar na si hilo tu pia tunahusika kumpa stahiki zake zote ikiwemo matibabu.

“Kwa kawaida pindi kiongozi yoyote wa kitaifa anapokuwa Dar es Salaam na kama hana nyumba SMZ hulipa malazi ya kiongozi wake na Maalim bado ni kiongozi na hata kama akiondoka kwenye uongozi bado anazo stahiki zake ikiwemo kuhudumiwa kama kiongozi mstaafu,” alisema Waziri Aboud.

Alisema pamoja na hali hiyo kwa sasa Serikali ya Muungano ndiyo inayolipa gharama za Maalim Seif kuishi hotelini kwa agizo la Rais Dk. John Magufuli.

Alisema ahadi ya Rais Magufuli ya kusaidia kulipia hoteli anayoishi Maalim Seif inaonesha ni namna gani Serikali zote mbili ya Muungano na ile ya Zanzibar zinavyoshirikiana kwa dhati.

“Kwa ubinadamu wake Rais Magufuli tunamshukuru sana kwani inaonesha namna gani kiongozi huyo wa Jamhuri ya Muungano alivyo na mapenzi mema  na Zanzibar pamoja na viongozi wake.

“… ila pamoja na yote SMZ bado ina wajibu wa kutekeleza wajibu wake wa kuwatunza viongozi wake wote wakiwemo waliokuwa ndani ya Serikali pamoja na wale waliostaafu,” alisema Aboud.

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata