WALIOKUFA KATIKA AJALI YA BASI LA LUHUYE WAFIKA 17.


Idadi ya abiria waliokufa kutokana na ajali ya basi la Kampuni ya Luhuye katika Wilaya ya Busega, mkoani  Simiyu juzi imeongezeka kutoka 12 hadi 17.

Baadhi ya marehemu, akiwamo Mchungaji wa Kanisa la Waadiventista Wasabato (SDA) Wilaya ya Kahama, mkoanim Shinyanga, wametambuliwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo, alisema wawili kati yao, walifariki  juzi jioni wakati wakiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Bugando.

Hata hivyo, Kamanda Mkumbo alisema Jeshi la Polisi linamshikilia mmiliki wa basi hilo, Masalu Jackson (37)mkazi wa eneo la Majengo mapya, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara,  kwa ajili ya upelelezi wa kipolisi.

Kwa mujibu wa Kamanda Mkumbo, baadhi ya maiti na majeruhi bado hawajatambuliwa hadi kufikia jana jioni.

Aliwataja maiti waliotambuliwa kuwa ni Mchungaji huyo wa SDA, Thomas Mwita (40), naAfisa Elimu wa Shule Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Mkoa wa Shinyanga, Wangwe Maurice ( 30), ambao walikuwa wakitibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Magu.

Aliwataja wengine,  ambao pia walikuwa  wakitibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Magu  kuwa ni Mahemba Chacha (42), mkazi  wa Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara, Rahma  Kibera (32) mkazi wa Bugalika, jijini Mwanza, Alex  Masatu (42).

Ingawa hakutaja majina, Kamanda Mkumbo alisema majeruhi tisa waliokuwa   wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Magu wametambuliwa na kwamba, wawili kati yao,  hali zao ni mbaya.

“Majeruhi 33 waliofikishwa Hospitali ya Rufaa Bugando kwa ajili ya matibabu, bado  wamelazwa. Wengine wawili, Esther Moris (18) mkazi wa Sirari, wilayani Tarime, mkoani Mara na Rose Wilson (21) mkazi wa Igoma, jijini Mwanza walifariki jana jioni  baada ya kuwa nimetoa taarifa za awali kwa vyombo vya habari,” alisema.

Aliwataja wengine waliokufa jana wakati wakitibiwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando  kuwa ni Sheta Msongoma (58), mkazi wa Nassa, Jimbo la Busega, mkoani Simiyu na mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja, Baraka Alex.

“Tusaidiane kutoa wito kwa watu wa mbali wajitokeze kwa wingi katika hospitali hizi mbili; Magu na Bugando ili wawatambue ndugu zao,”  alisema Kamanda Mkumbo.

KIKWETE ATUMA RAMBIRAMBI
Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Paschal Mabiti, kufuatia vifo vya watu 17 waliopoteza maisha yao katika ajali ya basi hilo.

Katika salamu hizo, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuwa ajali za barabarani zinaendelea kuchukua maisha ya watu wasiokuwa na hatia.

“Nimepokea kwa huzuni nyingi taarifa ya ajali hiyo ambayo nimejulishwa kuwa imetokea katika kijiji cha Itwimila katika Wilaya ya Busega katika Mkoa wako wa Simiyu wakati basi lililokuwa linasafiri kutoka Tarime, Mkoa wa Mara kwenda Mwanza kupitia Simiyu lilipoacha njia na kugonga nyumba kabla ya kupinduka.”

“Nakutumia salamu zangu za rambirambi na najiunga nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa katika nchi yetu. Aidha, kupitia kwako, natuma salamu za dhati ya moyo wangu kwa familia zote ambazo zimepoteza wapendwa wao katika ajali hiyo.

Naungana nao katika kuomboleza wapendwa wao. Napenda wajue kuwa msiba wao ni msiba wangu. Pia, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aziweke peponi roho za marehemu, alisema Rais Kikwete.”

Pia Rais Kikwete ametoa pole kwa wote ambao wameumia katika ajali hiyo, akiwaombea wapone haraka na kurejea kwenye shughuli zao za kujiletea maendeleo.
MATUKIO KATIKA PICHA HOSPITALI YA BUGANDO:
DR DERICK DAVID AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI
Ongezeko la majeruhi hospitalini hapo limesababisha msongamano kiasi cha kusababisha wagonjwa kulazwa wawili wawili kwenye vitanda. 
Huku akieleza kuwa hajui amefikaje katika Hospitali ya Bugando majeruhi ajali ya basi Yohana Peter Milinde akizungumza kuhusu anachokikumbuka mara ya mwisho,
wodini
Mungu awape ahuheni mpone haraka ndugu zetu.MANESI WAKIWA KATIKA PIRIKAPIRIKA ZA KUWAHAMISHA WAGONJWA.
majeruhi baada ya kupata matibabu
Majeruhi wa ajali ya basi Peter Funga naye amelaumu vitendo vya baadhi ya madereva kutozingatia kanuni na sheria zinazowaongoza barabarani hata kusababisha ajali.  
SOURCE:NIPASHE 

SAMBAZA HABARI HII
Habari Iliyopita
Habari Inayofuata