TUNDU LISSU AMEPELEKWA NYUMBANI KWAKE KUPEKULIWA

TUNDU LISSU AMEPELEKWA NYUMBANI KWAKE KUPEKULIWA
Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amepelekwa nyumbani kwake na Polisi kwa ajili ya kupekuliwa.

Tundu Lissu anashikiliwa na Polisi baada ya kummakata jana alipokuwa anatoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo alipelekwa Kituoni kuhojiwa kwa makosa mawili. 
Kosa la kwanza ni kumkashifu Rais, na kosa la pili ni la uchochezi dhidi ya ndege za serikali kuzuiwa Canada

SERIKALI KUONDOA MFUMO WA ZAMANI WA MALIPO YA KODI YA ARDHI

SERIKALI KUONDOA MFUMO WA ZAMANI WA MALIPO YA KODI YA ARDHI
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikishirikiana na Wizara ya Fedha, imesambaza maafisa wake katika halmashauri 169 kote nchini.

Maafisa hawa wanaotoa mafunzo katika vituo vyote vya makusanyo ya kodi ya ardhi na tozo nyingine kwa kutumia simu ya mkononi ili kuondoa kabisa mfumo wa zamani wa malipo.

Zaidi ya maafisa 170 kutoka makao makuu ya Wizara ya Ardhi, Wizara ya Fedha na kutoka kanda nane za ardhi wameanza kutoa elimu hiyo katika halmashauri na vituo vyote vya makusanyo ya kodi ya ardhi ili kurahisisha ulipaji kodi ya ardhi kwa wananchi kwa kutumia simu zao na kuondoa usumbufu.

Mfumo wa ulipaji kodi ya pango la ardhi kwa njia ya simu ya mkononi ni mfumo wa kielektroniki wa Government electronic Payment Gateway (GePG) katika makusanyo ya kodi ya pango la ardhi ambao utamrahisishia mwananchi kulipia popote walipo kwa kutumia simu zao kwa urahisi zaidi.

Mwananchi yeyote anayemiliki kiwanja au shamba lililopimwa na kupatiwa hati, ataweza kutumia simu yake ya mkononi kujua kiasi cha kodi ya pango la ardhi anachodaiwa na kukulipa kwa kutumia simu yake ya mkononi.

Ili kujua unadaiwa kiasi gani cha kodi ya pango la ardhi kwa kutumia simu ya mkononi bonyeza *152*00# au kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi yaani sms halafu unatuma kwenda namba 15200 na baada hapo unaweza kulipia kwa njia ya Mpesa, Tigo Pesa au kulipia tawi lolote la benki ya NMB na CRDB.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza rasmi kutumia mfumo huu wa kielektroniki wa GePG katika makusanyo ya kodi ya pango la ardhi pamoja na tozo nyingine zinazotokana na sekta ya ardhi nchini na kuondoa kabisa mfumo wa zamani.

Mfumo huu utamrahisishia mwananchi kulipa kodi ya pango la ardhi popote alipo, ikiwa ni pamoja na kulipia tozo nyingine mbalimbali za sekta ya ardhi. Mmiliki wa kipande cha ardhi ataweza kujua anadaiwa kiasi gani cha kodi ya pango la ardhi na kulipia popote alipo bila kusumbuka kufuata huduma hizo katika vituo vya makusanyo.

Kwa majaribio ya ukusanyaji kodi ya pango la ardhi kwa kutumia mfumo wa kielektroniki yalifanywa katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na baada ya mafanikio makubwa kuonekana elimu ikatolewa kwa watendaji wote wa sekta ya ardhi katika Halmashauri zote za mkoa wa Dar es salaam kabla ya zoezi hilo kuhamishiwa mikoani.

Kwa zile huduma nyingine za sekta ya ardhi ambazo zinahusisha malipo kama vile upekuzi katika daftari la msajili (official search), mwananchi atapaswa kutembelea ofisi za Wizara ya ardhi zilizo katika eneo lake na kupatiwa makadirio ya kulipia huduma husika pamoja na namba ya malipo itakayomuwezesha kulipia aidha kwa njia ya benki au simu ya mkononi.

Kwa sasa kikosi kazi kinachotoa mafunzo juu ya matumizi ya mfumo huu kimeshaanza kuelemisha mikoa mingine baada ya kupata mafanikio mazuri katika mkoa wa Dar es Salaam. Lengo kubwa la kutumia mfumo huu ni kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa maduhuli ya serikali pamoja na kurahisisha ulipaji kodi ya pango la ardhi nchini.

WAZIRI NCHEMBA ATISHIA KUWAFUTIA URAIA WATANZANIA WABAGUZI

WAZIRI NCHEMBA ATISHIA KUWAFUTIA URAIA WATANZANIA WABAGUZI
Waziri wa mambo ya ndani Mh. Mwigulu Nchemba ametishia kuwafutia uraia watanzania wapya wa Katumba mkoani Katavi ambao walikuwa wakimbizi kwa muda mrefu kutokana na tabia ya ya baadhi yakubaguana kitaifa na kikanda.

Waziri Nchemba amesema hayo jana  wakati  alipopita kwenye kambi kuangalia usajili unaendeleaje ambapo amesema  wananchi   hao waliopewa uraia wakitokea burundi wakati wa vita ya kikabila miaka 1972 wamekuwa na tabia ya ubaguzi hata kufikia kushindwa kusaidiana kwenye biashara zao.

Waziri aliwaambia wananchi hao kuwa yeyote atakayeleta mambo ya ubaguzi ikiwa ni pamoja na kubaguana kibiashara  katika jamii hatosita kumfutia uraia alioupata kwani Watanzania hawana mambo ya kibaguzi.

Pamoja na hayo Kiongozi huyo alitumia muda huo kuwataka Watanzania kuwa na utanzania ndani ya mioyo yao na waache tabia ya kutaka kukwamisha kila kitu kinachofanywa na serikali kwa kuweka vikwazo mbele ili vitu visifanikiwe.

SERIKALI KUNUNUA RADA 4 ZA KISASA

SERIKALI KUNUNUA RADA 4 ZA KISASA
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga (TCAA) jana (Jumanne) imeingia makubaliano na kampuni    inayojihusisha na mifumo ya anga kutoka nchini Ufaransa ya Thales kununua rada mpya nne.

Tukio hilo lilishuhudiwa na Waziri wa Ujenzi uchukuzi na mawasiliano Profesa Makame Mbarawa  na wadau wengine wa usafiri wa anga nchini. 
Upande wa Serikali mkataba ulisainiwa na Mkurugenzi wa Mkuu wa TCAA Hamza Johari na upande wa Thales alikuwa ni Meneja wa masoko wa kanda kutoka kampuni ya Thales Abel Aberr Carr.

Mkurugenzi wa Mkuu wa TCAA Hamza Johari anasema kwa sasa Tanzania ina rada moja pekee na uwezo wake kiufanisi umepungua kutokana na mabadiliko yanayotokea kwa haraka katika sekta hiyo, sanjari na kuongezeka kwa ndege zinazotumia anga la nchi.

“Mradi wa rada hizo ni miongoni mwa mipango mikakati iliyopewa kipaumbele cha juu na menejimenti ya TCAA kwa lengo la kuboresha huduma za uongozaji wa ndege kwa haraka, tija na kuongeza usalama katika sekta ya usafirishaji wa anga nchini na duniani,” amesema Johari.

Kwa upande wake Profesa Mbarawa amesema kufungwa kwa rada hizo kutaongeza imani ya wadau wa sekta ya usafiri wa anga dunia kuwa na imani na kutumia anga la Tanzania, hivyo watalii wataongezeka kwakuwa wanajua usafiri wa anga nchini kwetu ni wa usalama.

 “Kupatikana kwa rada hizo mpya tutaweza kutoa huduma kwa ndege nyingi zaidi na kulitawala anga letu zima. Ndege zikiongezeka na watalii wakaongezeka uchumi wetu utapiga hatua” alisema Profesa Mbarawa. 

Aidha kabla ya tukio hilo Waziri Mbarawa alitembelea chuo cha usafiri wa anga (CATC) ambapo alikutana na changamoto ya ufinyu wa eneo la chuo, ufinyu wa bajeti ya kununulia vifaa vya mafunzo na upungufu wa wataalamu.

ALICHOJIBU POLEPOLE BAADA YA KUAMBIWA VIATU VYA NAPE VINAMPWAYA

ALICHOJIBU POLEPOLE BAADA YA KUAMBIWA VIATU VYA NAPE VINAMPWAYA
Kupitia kwenye account yake ya twitter Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Humphrey Polepole ametoa majibu kwa Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa akimwambia kuwa hatokuwa tena Mbunge baada ya Awamu hii.

Hatua hiyo ya Polepole imekuja baada ya kuambiwa na Mbunge Msigwa kuwa viatu vya Nape havimtoshi kupitia twitter ambapo aliandika; "Kitendo cha Msukuma kumkumbuka Nape , ni ujumbe tosha Kuwa Viatu vya Nape vinampwaya POLEPOLE!"

Baada ya ujumbe huo naye Polepole kupitia twitter aliandika; "Kitu kimoja nakuahidi, hii ni term yako ya mwisho, tunakurudisha kufanya kazi ya Uchungaji maana naona mchungaji anajichanganya na mbuzi."

PANYA WAMUHAMISHA RAIS IKULU......SASA KUFANYIA KAZI NYUMBANI

PANYA WAMUHAMISHA RAIS IKULU......SASA KUFANYIA KAZI NYUMBANI
Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari, atalazimika kufanyia kazi zake akiwa nyumbani baada ya panya kuharibu ofisi yake iliyopo Ikulu.

Msemaji wa Rais Buhari, Garba Shehu, amesema, panya hao wameharibu samani za viyoyozi katika ofisi hiyo hivyo kiongozi huyo hawezi kufanya kazi katika ofisi mbovu ambayo itakarabatiwa kwa kipindi cha miezi mitatu.

Bw. Garba amesema, hatua ya Rais Buhari kufanyia kazi zake nyumbani hakutaathiri ufanisi wake kwa aina yoyote ile.

Rais Buhari alirejea nyumbani Nigeria Jumamosi iliyopita baada ya kukaa Jijini London nchini Uingereza kwa zaidi ya siku 100 alikokuwa akipatiwa matibabu kwa ugonjwa ambao hata hivyo haujawekwa wazi.